Friday, August 9, 2024

RUTO AWAAPISHA MAWAZIRI NUSU NI MAWAKILI

 


Rais Ruto Awaapisha Mawaziri Wapya, Zaidi ya Nusu Wakiwa Mawakili

Rais wa Kenya, William Ruto, leo Alhamisi amewaapisha mawaziri 19 aliowateua hivi karibuni, huku zaidi ya nusu yao wakitajwa kuwa mawakili. Kulingana na ripoti za mitandao ya kimataifa, mawaziri wanane kati ya walioapishwa wanashikilia Shahada za Uzamili na Sheria. Katika orodha hiyo, Mwanasheria Mkuu mteule, Dorcas Oduor, na Katibu wa Baraza la Mawaziri, Mercy Wanjau, nao pia ni mawakili, na hivyo kuongeza idadi ya mawakili katika Baraza jipya la Mawaziri la Rais Ruto kufikia kumi.

Uteuzi wa Rais Ruto unachukuliwa kama hatua ya kukabiliana na changamoto kadhaa za kisheria ambazo serikali yake imekumbana nazo katika kipindi cha miaka miwili tangu alipoingia madarakani. Madai haya yamezidi kuibuka, yakidokeza uwezekano wa ushauri usiofanikiwa wa kisheria kwa Rais na mawaziri wake.

Miongoni mwa mawakili walioteuliwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Profesa Kithure Kindiki, Waziri wa Ardhi, Kazi za Umma, Nyumba na Maendeleo ya Miji, Alice Wahome, Waziri wa Kawi na Petroli, Opiyo Wandayi, Waziri wa Elimu, Julius Ogamba, Waziri wa Ulinzi, Roselinda Tuya, Waziri wa Utalii, Rebecca Miano, Waziri wa Masuala ya Michezo na Vijana, Kipchumba Murkomen, na Waziri wa Utumishi wa Umma, Justin Muturi.

Katika hotuba yake wakati wa hafla hiyo, Rais Ruto alisisitiza dhamira yake ya "kutumia kikamilifu fursa zote ndani ya miundo na mifumo yetu ya kisheria na kitaasisi, ili kushirikiana na asasi za kitaifa za haki na sheria kwa lengo la kuongeza ufanisi katika uchunguzi wa kesi zote ndani ya muda uliowekwa."


0 comments: