Monday, July 22, 2024

KADI ZA MPIGA KURA ZA 2015 NA 2020 KUENDELEA KUTUMIKA.



Kadi za Mpiga Kura Zilizotolewa 2015 na 2020 Zitaendelea Kutumika Katika Chaguzi Kuu Zijazo

Kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zitaendelea kutumika katika chaguzi kuu zijazo, licha ya mabadiliko ya jina la Tume ya Uchaguzi kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi. Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Kailima Ramadhan, alibainisha haya alipokuwa akitembelea vituo vya kuandikishia wapiga kura leo tarehe 22 Julai, 2024, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kasulu.

Ramadhan alisema wapiga kura wenye kadi hizo hawahusiki na zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Alifafanua kwamba, "Naomba nitoe wito kwa wale ambao kadi zao ni zile zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wanadhania kuwa kubadilika kwa jina la Tume kunasababisha kubadili kadi watambue kuwa kadi zao ni halali kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024."

Ziara hiyo ya Mkurugenzi wa Uchaguzi iliambatana na Afisa Mwandikishaji wa Jimbo la Kasulu Vijijini, Emmanuel Ladislaus, pamoja na maafisa wengine waandamizi. Ramadhan alieleza kuwa wapiga kura wenye kadi ambazo zimeharibika, zimepotea, au wale ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine wanahusika kwenye zoezi hilo.

"Nimebaini kuwa wapo wapiga kura wenye kadi za zamani zilizotolewa kabla ya mwaka 2015 (zile za karatasi), hao waje vituoni ili waandikishwe upya kwa kuwa mfumo uliotumika wakati huo ni tofauti na mfumo wa sasa," alisema Ramadhan.

Aidha, Kailima aliwakumbusha wananchi wa mikoa ya Kigoma, Tabora, na Katavi kuwa zimebaki siku tatu kwa zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kukamilika kwenye mikoa yao. Uboreshaji huo ulianza tarehe 20 Julai, 2024, na utafanyika kwa siku saba hadi tarehe 26 Julai, 2024, ambapo vituo vinafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni. Wananchi wametakiwa kujitokeza kwa wingi na kutumia vizuri siku hizo.


 

0 comments: